Connect with us

Fainali ya mchezo wa soka kuwania ubingwa wa Afrika AFCON, huenda ikaanza kuchezwa mwezi Juni au Julai ikiwa mapendekezo haya yataidhinishwa na Mkutano mkuu wa Shirikisho la soka barani Afrika CAF.

Mapendekezo haya yamekuja baada ya kubainika kuwa wakati wa fainali hiyo mwezi Januari na Februari, wachezaji wengi wa Afrika huwa wanashindwa kujigawa au hata kuja kuchezea timu zao za taifa kwa sababu michuano ya ligi kuu barani Ulaya wanakocheza huwa zimeshika kasi.

Aidha, imependekezwa kuwa mataifa yanayoshiriki katika fainali hiyo iongezwe kufikia 24 kutoka 16.

Uamuzi wa mwisho utaamuliwa na wajumbe wanaokutana nchini Morocco siku ya Ijumaa, watakapopigia kura mapendekezo haya.

Rais wa Shirikisho la soka barani Afrika CAF Ahmad Ahmad amesema kuwa anaamini kuwa mabadiliko haya ni muhimu na yatasaidia kuimarisha soka barani Afrika.

Mbali na michuano baina ya timu za Afrika, huenda ratiba ya michuano ya klabu bingwa na Shirikisho barani Afrika ikabadilishwa.

Fainali ya michuano hii huwa inachezwa mwezi Novema kila mwaka. Mapendekezo haya ni ahadi iliyotolewa na Ahmad wakati akitafuta uongozi wa CAF mapema mwaka huu.

More in