Connect with us

Vlabu tano kutoka ukanda wa Afrika Mashariki na Kati CECAFA, vimefuzu katika hatua ya 32 bora kuwania taji la klabu bingwa barani Afrika, baada ya kumalizika kwa michuano ya hatua ya awali siku ya Jumatano.

Timu zilizofuzu katika hatua hiyo ni pamoja na Saint George ya Ethiopia na KCCA ya Uganda, ambazo zitamenyana katika hatua hii ya 32, katika mechi zitakazochezwa nyumbani na ugenini mwezi Machi.

Yanga ya Tanzania iliyocheza na Saint Loius United ya Ushelisheli, ilifuzu baada ya kupata ushindi wa jumla ya mabao 2-1, na sasa itamenyana na Township Rollers ya Bostwana.

Mabingwa wa soka nchini Kenya Gor Mahia, watakabiliana na Esperance de Tunis ya Tunisia, baada ya kufanikiwa kuishinda Leones Vegetarianos ya Equitorial Guinea kwa mabao 3-1.

Baada ya sare ya bao 1-1 nyumbani, Rayon Sports ya Rwanda ilijikakamua na kuishinda LLB Academic FC ya Burundi kwa jumla ya mabao 2-1, baada ya kupata ushindi muhimu ugenini wa bao 1-0 jijini Bujumbura.

Wawakilishi hao wa Rwanda sasa watamenyana na mabingwa wa mwaka 2016, Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.

Ratiba nyingine:-

TP Mazembe (DRC) v UD Songo (Msumbiji )

Difaa El Jadidi (Morocco) v AS Vita Club (DRC)

AS Togo-Port (Togo) v Al-Hilal (Sudan)

Hali ilikuwa hivyo kwa timu zinazopambana kuwania taji la Shirikisho msimu huu.

APR ya Rwanda baada ya kuishinda, Anse Reunion ya Ushelisheli kwa mabao 6-1, sasa itamenyana na Djoliba ya Mali katika hatua ya 32 bora.

Simba FC ya Tanzania, itachuana na Al-Masry ya Misri baada ya kuishinda Gendarmerie Nationale ya Djibouti kwa mabao 5-0.

Welayta Dicha ya Ethiopia, itamenyana na Zamalek ya Misri baada ya kushinda Zimamoto ya Zanzibar kwa jumla ya mabao 2-1.

Olympique Star ya Burundi, itamenyana na Al-Hilal Al-Ubayyid ya Sudan.

Washindi watamenyana na timu 16, zitakazokuwa zimepoteza katika hatua ya mwondoano ya michuano ya klabu bingwa, ili kupata timu 16 bora kwenda katika hatua ya makundi.

Ratiba nyingine:-

AS Maniema Union (DRC) v USM Alger (Algeria)

DC Motema Pembe (DRC) v Deportivo Niefang (Equitorial Guinea)

CS La Mancha (Congo) v Al-Ahly Shendi (Sudan)

More in East Africa