Connect with us

CHAN 2016: Wenyeji Rwanda waanza kwa ushindi dhidi ya Cote D’ivore

CHAN 2016: Wenyeji Rwanda waanza kwa ushindi dhidi ya Cote D’ivore

Makala ya nne ya michuano ya CHAN barani Afrika, kwa wachezaji wanaocheza soka nyumbani yameanza rasmi jioni hii jijini Kigali nchini Rwanda.

Mchuano wa ufunguzi ukiwa ni kati ya wenyeji Amavubi Stars ya Rwanda na Tembo kutoka Cote D’voire katika uwanja wa Amahoro jijini Kigali.

Maelfu ya mashabiki walihudhuria mchuano huo wa ufunguzi ambao ulimalizika kwa Rwanda kushinda kwa bao 1 kwa 0 kupitia mchezaji Bayisenge Emery katika dakika ya 16 kipindi cha kwanza kupitia mkwaju wa adhabu “Free-kick”.

Kipindi cha pili, Rwanda ilipoteza nafasi ya kuongeza bao baada ya mfungaji wa bao la kwanza Bayisenge Emery kupoteza mkwaju wa penalti, baada ya nahodha Jacques Tuyisenge kuangushwa na mabeki wa Cote Cote D’voire katika eneo la hatari.

Cote Divoire, ilijitahidi kutawala kipindi cha pili na kupata nafasi katika dakika ya 89, baada ya Djedje Guiza kupiga shuti iliyogonga mwamba na kuinyima Tembo nafasi ya kusawazisha bao.

Baadaye usiku, katika mchuano mwingine wa kundi A, Gabon watamenyana na Morroco kuanzia saa moja kamili usiku saa za Afrika Mashariki katika uwanja wa Amahoro.

Kesho Jumapili ni michuano ya kundi B, mabingwa wa kwanza kabisa wa mashindano haya Leopard ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo iliyoshinda taji hili mwaka 2009, itafungua dimba dhidi ya Walia Ibex ya Ethiopia katika uwanja wa Huye mjini Butare.

Angola nao watachuana baadaye na Cameroon kuanzia saa moja jioni katika mchuano mwingine wa kundi hilo.

Serikali ya Rwanda imetumia Dola Milioni 21 nukta 4 kuandaa makala haya ya nne ya CHAN, na imeondoa ada ya Visa kwa mashabiki na wachezaji kutoka mataifa 15 yanayoshiriki katika mashindano haya kuja kushuhudia michuano hii kwa wingi.

Mataifa 16 yanayoshiriki katika michuano hii ni pamoja na:-

  • Kundi la A: Gabon, Ivory Coast, Morocco na wenyeji Rwanda.
  • Kundi la B: Angola, Cameroon, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Ethiopia
  • Kundi C: Guinea, Niger, Nigeria na Tunisia
  • Kundi la D: Mali, Uganda, Zambia na Zimbabwe.

Takwimu muhimu kuhusu historia ya CHAN:

  • Ivory Coast ilikuwa nchi ya kwanza kuwa wenyeji wa michuano hii mwaka 2009, Sudan walikuwa wenyeji mwaka 2011 huku Afrika Kusini ikiwa mwenyeji mwaka 2014.
  • Kenya itakuwa mwenyeji wa mashindano ya mwaka 2018.
  • DRC ilishinda Ghana mabao 2 kwa 0 katika fainali ya mwaka 2009
  • Tunisia iliifunga Angola mabao 3 kwa 0 katika fainali ya mwaka 2011
  • Libya iliishinda Ghana mabao 4 kwa 3 baada ya sare ya kutofungana katika muda wa kawaida mwaka 2014 wakati michuano hii ilipofanyika nchini Afrika Kusini.
  • DR Congo na Zimbabwe ndio mataifa pekee ambayo yameshiriki makala yote manne ya mashindano haya ya CHAN tangu kuzinduliwa.
  • Cameron na Tunisia hazijawahi kupoteza mchuano wowote katika hatua ya makundi katika michuano hii, lakini Zimbabwe imekuwa na sare nyingi zaidi.
  • Ethiopia walishiriki kwa mara ya kwanza mwaka 2014 na Rwanda mwaka 2011 na katika michuano hiyo hazikupata ushindi katika mchuano wowote.
  • Mchezaji kutoka Zambia Given Singuluma anaendelea kushikilia rekodi ya kuwa mfungaji bora katika historia ya mashindano haya na mwaka 2009 alifunga mabao 5.
  • Guinea ndio timu ya pekee inayoshiriki katika michuano hii kwa mara ya kwanza.

 

 

Bedjos Solutions Bondo

Must See

More in