Connect with us

Changamoto za watangazaji wa kisasa wa soka kupitia redio

Changamoto za watangazaji wa kisasa wa soka kupitia redio

Na Victor Abuso,

Hapana shaka kuwa, siku za hivi karibuni vijana wengi wamejitosa katika utangazaji wa soka kupitia redio katika nchi za Afrika Mashariki na Kati.

Hili ni jambo zuri sana na la kutia moyo kwa kizazi hiki.

Licha ya kazi hii inayoelekea kuenziwa na kupendwa na vijana walio na vipaji vya utangazaji, inahitaji pia uzoefu na ufundi wa kipekee ili kuifanya vizuri.

Ukiwasikiliza watangazaji wa kisasa na wale wa zamani, hasa barani Afrika kwa kweli kuna tofauti kubwa sana ya namna wanavyofanya kazi hii.

Changamoto ya kwanza inayowakumba watangazaji wa kisasa, ni kutofahamu historia ya wachezaji, klabu au timu ya taifa husika na takwimu mbalimbali. Hii imewanyima wasikilizaji na wapenzi wa soka ufahamu wa kina kuhusu wachezaji na timu hizo.

Ukiwasikiliza baadhi ya watangazaji chipukizi, huwezi kupata historia ya mchezaji, nikiwa na maana alizaliwa lini na wapi, alicheza wapi na maendeleo yake ya hivi karibuni, amefunga mabao mangapi na mambo kama hayo. Hiki kinakosekana siku hizi.

Matumizi yasiyofaa ya lugha pia ni tatizo lingine. Watangazaji wengi wa siku hizi wanapenda sana kuchanganya lugha jambo ambalo linawachanganya wasikilizaji.

Mfano mtangazaji anasema, “ Mchezaji anachukua mpira, anapiga Cross na Ball imetoka nje,”. Hapa amechanganya Kiswahili na Kiingereza mfumo ambao unamchanganya mtu wa kawaida anayefuatilia matangazo.

Watangazaji kama Jack Oyoo Silvester, Leonard Mambo Mbotela, Ali Sali Manga wote kutoka Kenya, Charles Hillary kutoka Tanzania ni wakongwe wanaotumia lugha moja. Wanatumia Kiswahili na hakuna siku utawasikia wakichanganya lugha.

Barani Ulaya, watangazaji wa huko hutumia Kiingereza pekee ikiwa wapo katika nchi zinazozungumza lugha hiyo sawa na Kifaransa katika nchi zinazozungumza lugha hiyo. Hawawezi kuchanganya lugha hiyo kwa lengo la kutaka msikilizaji aelewe. Hapa kwetu hili bado ni tatizo.

Changamoto nyingine muhimu na ya tatu ni mwendo unaotumiwa kutangaza mechi husika.

Sisemi haifai kuonesha uchangamfu lakini ni vema kuwa makini usisikike kana kwamba unaimba badala ya kuzungumza.

Siku zote ni muhimu kukumbuka kuwa watu wa rika, na makundi mbalimbali wanakusikiliza na lengo lako ni kuhakikisha kuwa wanakuelewa.

Mwendo wa kasi sana sio mzuri.Wengi watakosa kuelewa kinachosemwa.

Naamini ni vizuri kuwa katika mwendo wa kati, usitangaze kwa haraka sana wala taratibu sana hadi watu wanaokusikiliza wasiinzie.

Baadhi ya watangazaji waliotia fora miaka ya 60,70 na 90 na ambao wanakumbukwa sana barani Afrika ni pamoja na Joe Lartey, Kwabena Yeboah wote kutoka Ghana, Ernest Okonkwo kutoka Nigeria , Dennis Liwewe kutoka Zambia na Zama Masondo kutoka Afrika Kusini.

Hawa ni watangazaji waliokuwa wakitangaza na kuwakusanya wasikilizaji katika vikundi kuwasikiliza na ungefikiri wanauona mchuano huo uwanjani.

Watangazaji wa sasa wanaweza kujifunza mengi kutoka kwa watangazaji hao wa zamani na kuwa bora zaidi ikiwa watakubali mapungufu yao na kuwa na moyo wa kupokea masahahisho

Ex- CAF Media Expert. An expert on African football with over 15 years experience ,always with an ear to the ground with indepth knowledge of the game. I have worked for top publications including 7 years at www.supersport.com until i founded www.soka25east.com to quench the thirst of football lovers across the continent. I have trained young upcoming journalists who are now a voice in African football.I have covered World Cup,AFCON,CHAN,Champions League,Confederations Cup,Cecafa,Cosafa,Wafu and many other football tournaments across the World. Founder Football Africa Arena(FAA),Founder www.afrisportdigital.com

Bedjos Solutions Bondo

Must See

More in