Connect with us

Klabu za AS Vita Club ya DRC, Renaissance Berkane ya Morocco na Al Masry zimefuzu katika hatua ya robo fainali, kuwania taji la Shirikisho barani Afrika.

Wakicheza nyumbani, Fabrice Ngoma na Jean-Marc Mundele waliifungia AS Vita Club mabao 2, dhidi ya Raja Casablanca ya Morocco na kujihakikishia kufika katika hatua hiyo.

Matokeo mengine yaliyowashangaza wengi, ilikuwa ni kati ya ASEC Mimosas ya Ivory Coast, iliyoishinda Aduana Stars ya Ghana mabao 2-0 ugenini.

Vita Club inaongoza kundi la A, kwa alama 10, ikifuatwa na Raja Casablanca ambayo ina alama nane.

Kundi B, tayari Berkane na Masry zimejihakikishia nafasi ya robo fainali, baada ya kuzishinda UD Songo ya Msumbiji na Al Hilal ya Sudan.

RS Berkane inaongoza kundi hili kwa alama 10, baada ya mechi mitano huku ikifuatwa na Al-Masry iliyo na alama 9.

CARA Brazaville ya Congo na Enyimba ya Nigeria nazo zinatafuta sare katika mechi ya mwisho tarehe 29 mwezi huu, ili kusonga mbele.

Williamsville AC ya Ivory Coast nayo ina nafasi iwapo itaishinda Djoliba ya Mlai, na kuomba kuwa mechi kati ya CARA Brazaville na Enyimba mechi hiyo ikitokea sare au mmoja amfunge mwingine.

Viongozi wa kundi D Gor Mahia ya Kenya, walipata matokeo ya kushtua baada ya kufungwa na Rayon Sport ya Rwanda mabao 2-1 jijini Nairobi.

Mabao ya Rayon yalifungwa na Bonfilscaleb Bimenyimana katika dakika ya tatu ya mchuano huo, huku Eric Rutanga akifunga bao la pili katika dakika ya 53 kupitia mkwaju wa adhabu, na kuwapa wawakilishi hawa wa Rwanda ushindi wa kwanza katika kundi hili.

Young Africans ya Tanzania nayo, ilipata ushindi wake wa kwanza wa mabao 2-1 dhidi ya USM Alger jijini Dar es salaam na kuwashangaza wageni hao.

Kuelekea mechi ya mwisho, Gor Mahia wanaongoza kundi hili kwa alama nane, mbele ya USM Alger ambayo pia ina alama hizo nane lakini inapungukiwa mabao.

Rayon Sport ambayo itamenyana na Young Africans katika mchuano wa mwisho jijini Kigali mwishoni mwa mwezi Agosti, inashikilia nafasi ya tatu kwa alama sita.

Mechi ya mwisho ya Gor Mahia watacheza na USM Alger.

 

More in