Connect with us

Klabu ya Gor Mahia ya Kenya imetetea taji la SportPesa, baada ya kuishinda Simba FC ya Tanzania mabao 2-0 katika fainali ya michuano ya mwaka huu ya SportPesa ambayo imekuwa ikichezwa katika uwanja wa Afraha nchini Kenya.

Mshambuliaji Meddie Kagere alikuwa wa kwanza, kuipa Gor Mahia bao la kwanza mwanzoni mwa mchuano huo, uliohudhuriwa na maelfu ya mashabiki wa Gor ambao ni mabingwa wa soka nchini humo.

Wachezaji wa Gor Mahia waliutawala mchezo huo, hasa safu ya kati huku Simba ambao ni mabingwa wa soka nchini Tanzania wakionekana kuchoka mapema wakati wote wa mchuano huo.

Shambulizi la Jacques Tusiyenge, katika kipindi cha pili cha mchuano huo, liliwamaliza wachezaji wa Simba walionekana kukata tamaa na kufanya matokeo kuwa 2-0.

Gor Mahia pamoja na taji hilo, imejishindia Dola 30,000 kutoka kwa SportPesa ambayo inafadhili soka nchini Kenya na Tanzania.

Kogalo kama inavyofahamika, sasa itakwenda nchini Uingereza mwezi ujao kucheza na Everton katika mchuano wa Kimataifa wa kirafiki katika uwanja wa Goodison Park, mjini Liverpool.

Singida United ya Tanzania ilimaliza katika nafasi ya tatu ya michuano hiyo.

Timu zingine zilizoshiriki ni pamoja na Yanga na JKU kutoka Tanzania na Kakamega HomeBoyz na Kariobangi Sharks zote za Kenya.

More in African Football