Connect with us

Klabu ya KCCA ya Uganda ndio timu pekee kutoka ukanda wa Afrika Mashariki iliyofuzu katika hatua ya makundi, kuwania taji la klabu bingwa barani Afrika.

KCCA ilifanikiwa baada ya kupata ushindi muhimu nyumbani wa bao 1-0 dhidi ya Saint George ya Ethiopia mwishoni mwa wiki iliyopita kupitia bao la Muhammad Shaban katika dakika ya 47 ya mchuano huo.

Mchuano wa kwanza, uliochezwa jijini Addis Ababa, timu zote mbili zilimaliza mchuano huo kwa kutofungana.

Kocha wa KCCA, ambao ni mabingwa wa soka nchini Uganda Mike Mutebi, amesema lengo la klabu yake ni kufika katika hatua ya robo fainali.

Klabu hii imekuwa ya kwanza kufuzu katika hatua ya makundi, kuwania taji la klabu bingwa Afrika.

Kikosi cha KCCA:-Charles Lukwago (Kipa), Dennis Okot Oola, Habibu Kavuma, Timothy Dennis Awany (Captain), Isaac Kirabira, Paul Mucureezi (85′ Solomon Okwalinga), Muzamiru Mutyaba, Allan Okello (66′ Julius Poloto), Mustapha Kizza, Muhammed Shaban (90′ Patrick Kaddu), Derrick Nsibambi

Gor Mahia ya Kenya, Yanga ya Tanzania, Al-Hilal ya Sudan na Rayon Sport ya Rwanda ni klabu za Afrika Mashariki ziliondolewa katika michuano hiyo na kupelekwa katika hatua ya Shirikisho.

Wachambuzi wa soka wanasema, kuanza vibaya nyumbani kwa timu za Afrika Mashariki kunaelezwa ndio sababu ya kuondolewa katika michuano hii.

Klabu zilizofuzu katika hatua ya makundi ni pamoja na:-

KCCA (Uganda), Mamelodi Sundowns (Afrika Kusini), Difaa El Jadidi (Morocco), Zesco (Zambia), AS Togo (Togo), Etoile du Sahel (Tunisia), Esperance (Tunisia), ES Setif (Algeria), Primeiro de Agosto (Angola), TP Mazembe (DRC)Township Rollers (Botswana), Horoya (Guinea), MC Alger (Algeria), Al Ahly (Misri), Wydad (Morocco) na Mbabane Swallows (Swaziland).

Droo ya hatua ya makundi itafanyika tarehe 21 mwezi Machi.

Shirikisho la soka barani Afrika CAF limesema kuwa Dola 550,000  zitatolewa kwa kila klabu iliyofika katika hatua ya makundi.

More in East Africa