Connect with us

Burundi na Kenya zilianza vizuri michuano ya kuwania taji la Afrika Mashariki CECAFA kwa upande wa wanawake.

Michuano hii ya kipekee ilianza mwishoni mwa wiki iliyopita katika Taasisi ya Njeru mjini Jinja nchini Uganda.

Burundi ilipata ushindi mkubwa wa mabao 10-1 dhidi ya Zanzibar katika mchuano wa kwanza ulianza kuchezwa kuanzia saa nane mchana saa za Afrika Mashariki.

Kufikia kipindi cha mapumziko, Burundi ilikuwa inaongoza kwa mabao 6-1, yaloyofungwa na Djazilla Uwimeza , Aziza Misigiyimana, Bukuru Joe’lle, Neilla Uwimana na Maggy Mumezero.

Mambo yalikuwa mabaya zaidi ya Zanzibar baada ya kipa wao Amina Mohamed Kitambi kupewa kadi nyekundu na kuondolewa uwanjani baada ya kuudaka mpira katika eneo lisilo sahihi.

Nayo timu ya taifa ya Kenya, inayofahamika kama Harambee Starlets ilianza vema michuano hii baada ya kuifunga wenyeji Uganda mabao 4-0.

Starlets ambayo inajiandaa kushiriki katika michuano ya Afrika nchini Cameroon, kati ya mwezi Novemba na Desemba mwaka huu, walionesha uwezo mkubwa wa kumiliki mpira mbele ya majirani zao.

Ratiba.
Jumatatu Septemba 12 2016

  • Tanzania vs Rwanda

Jumanne Septemba 13 2016

  • Burundi vs Kenya
  • Zanzibar vs Uganda

Jumatano Septemba 14 2016

  • Rwanda vs Ethiopia

Alhamisi Septemba 15 2016

  • Kenya vs Zanzibar
  • Uganda vs Burundi

Mechi za nusu fainali zitachezwa siku ya Jumamosi, Septemba tarehe 17 huku fainali ikipigwa siku ya Jumatatu tarehe 19.

Michuano hii inachezwa kwa mara ya pili kwa muda mrefu baada ya Zanzibar kuandaa michuano hii kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1986.

More in East Africa