Connect with us

East Africa

Kimanzi apewa tena Harambee Stars

Kimanzi apewa tena Harambee Stars

Francis Kimanzi ameteuliwa tena kuwa kocha wa timu ya taifa ya soka ya Kenya, Harambee Stars kwa mara ya tatu ndani ya miaka 10.

Kimanzi raia wa Kenya, mwenye umri wa miaka 43, anachukua nafasi ya Mfaransa Sébastien Migné aliyefutwa kazi baada ya Kenya kuondolewa na Tanzania katika michuano ya kufuzu kucheza fainali ya CHAN mwaka 2020 nchini Cameroon.

Mchezaji huyo wa zamani wa klabu ya Mathare United, atasaidiana na mzawa mwingine Zedekiah ‘Zico’ Otieno, na sasa wana kazi kubwa ya kuiongoza Kenya kufuzu kucheza fainali ya mataifa bingwa barani Afrika mwaka 2021 nchini Cameroon.

Pamoja na hilo, Kimanzi ana kibarua cha kuiongoza Kenya kufuzu kwa mara ya kwanza, katika fainali ya kombe la dunia nchini Qatar mwaka 2022.

Rais wa Shirikisho la soka nchini Kenya FKF Nick Mwendwa, amesema anawaamini makocha hao wa nyumbani, wataisadia Kenya, kutetea taji la CECAFA, wakati michuano ya mwaka huu itakapofanyika jijini Kampala nchini Uganda, mwezi Desemba.

Kumsaidia kuanza kuteua kikosi chake, FKF imetangaza kuwa, mwezi Septemba, Kenya itacheza mechi mbili za kimataifa za kirafiki dhidi ya Uganda na Libya.

“Nafahamu kuwa atafanikiwa. Makocha wa nyumbani barani Afrika, wamethibitisha kuwa wanaweza kufanya kazi nzuri na ndio sababu namwamini Kimanzi na Zico,” alisema Mwendwa.

Wawili hao wametia saini mkataba wa miaka miwili.

Kimanzi amerejea kuifunza Harambee Stars mara ya tatu, baada ya kufanya hivyo kwa mara ya kwanza mwaka 2008 na kufutwa kazi mwaka mmoja baadaye baada ya kutofautiana na viongozi wa soka wakati huo.

Mwaka 2011 aliteuliwa tena laini akafutwa kazi mwaka 2012, baada ya kushindwa kuisaidia Kenya kufuzu katika fainali ya mataifa bingwa barani Afrika mwaka 2013.

Mbali na Harambee Stars, wamekuwa kocha wa klabu ya Mathare United, Sofapaka na Tusker FC.

Kimanzi ameendelea kuwa na msimamo wa kupinga, makocha Wazungu kufunza soka barani Afrika.

Must See

More in East Africa