Connect with us

Kocha wa Cameroon aachishwa kazi

Kocha wa Cameroon aachishwa kazi

Shirikisho la soka nchini Cameroon limemfuta kazi kocha wa timu ya taifa, Volke Finke.

Hatua hiyo ilichukuliwa baada ya kikao cha Kamati kuu ya Shirikisho hilo siku ya Ijumaa kutokana na matokeo mabaya ya timu ya taifa.

Finke mwenye umri wa miaka 67 raia wa Ujerumani, amekuwa akiifunza Cameroon tangu mwaka 2013 na kikosi chake hakikuwa na matokeo mazuri wakati wa michuano ya kombe la dunia mwaka 2014 nchini Brazil na fainali za taji la mataifa bingwa barani Afrika mwaka 2015 nchini Equitorial Guinea.

Shirikisho la soka nchini humo Fecafoot limemteua Alexandre Belinga kuwa kocha wa muda na atasaidiana na Djonkep Bonaventure..

Kazi kubwa ya kocha huyo mpya ni kuiongoza Cameroon kufuzu katika fainali za kombe la dunia mwaka 2018 na mchuano wake wa kwanza utakuwa dhidi ya Niger tarehe 13 na 17 mwezi Novemba.

Cameroon ambao wakati mmoja walikuwa miamba wa soka barani Afrika, wameshindwa kurejea katika hali yao ya kawaida kama ilivyokuwa miaka mitano iliyopita.

Must See

More in