Connect with us

Ubelgiji imekuwa timu ya kwanza kutoka nyuma, baada ya kufungwa mabao 2-0 na kushinda mchuano muhimu wa kufuzu hatua ya robo fainali kuwania taji la kombe la dunia.

Hii ilidhihirika siku ya Jumatatu usiku, baada ya kuifunga Japan mabao 3-2 katika mchuano wa hatua ya 16, uliochezwa katika uwanja wa Rostov Arena.

Mara ya mwisho kuwa na matokeo kama haya wakati wa michuano ya mwondoano, ilikuwa ni mwaka 1970 wakati Ujerumani Magharibi, iliyokuwa imefungwa mabao 2-0 na Uingereza, ilipofanikiwa kumaliza mechi hiyo kwa ushindi mabao 3-2.

Japan ilioneka, katika kipindi cha pili kuwa ingeshinda mechi hiyo baada ya kupata mabao kutoka kwa Genki Haraguchi na Takashi Inui, lakini mambo yalibadilika baada ya Ubelgiji kufunga bao la kwanza kupitia Jan Vertonghen na Marouane Fellaini akasawazisha.

Mambo yalikuwa mabaya zaidi kwa Japan baada ya Nacer Chadli kufunga bao la ushindi katika dakika ya tisini ya mchuano huo na kudidimiza matumaini yao ya kuishangaza Ubelgiji.

Ubelgiji ambayo haijawahi kushinda kombe la dunia, itamenyana na mabingwa mara tano Brazil katika mchuano wa robo fainali siku ya Ijumaa, katika uwanja wa Kazan.

Mechi nyingine ya robo fainali, itakuwa pia siku ya Ijumaa kati ya Ufaransa na Uruguay katika uwanja wa Nizhny Novgorod.

Siku ya Jumamosi, wenyeji Urusi watamenyana na Croatia katika uwanja wa Olimpiki mjini Sochi.

Mechi za mwisho kutafuta timu mbili zitakazofuzu katika hatua ya robo fainali zinachezwa siku ya Jumanne.

Sweden itamenyana na Uswizi, huku Colombia ikicheza na Uingereza.

Washindi watakutana katika hatua ya robo fainali siku ya Jumamosi.

More in