Connect with us

Mkutano Mkuu wa viongozi wa  vyama vya soka barani Afrika utafanyika siku ya Jumapili mjini Sharm El Sheikh, nchini Misri.

Pamoja na mambo mengine kuhusu maendeleo ya mchezo huo,  viongozi hao kutoka mataifa zaidi ya 50 wakiongozwa na rais wa CAF Ahmad Ahmad, watashuhudia kupigwa kura ili kumchagua mjumbe kutoka Mataifa yanayozungumza lugha ya Kiingereza kuketi katika Baraza la Shirikisho la soka duniani FIFA.

Wanaowania nafasi hiyo ni pamoja na Danny Jordan (Afrika Kusini ),Leodegar Tenga(Tanzania), Elvis Chetty (Ushelisheli),Walter Nyamilandu (Malawi) na Nick Mwendwa(Kenya).

Mshindi atachukua nafasi ya Kwesi Nyantakyi aliyekuwa rais wa soka nchini Ghana na Makamu wa rais wa CAF, aliyejiuzulu kwa madai ya ufisadi na kufungiwa kushiriki katika masuala ya soka.

Kuelekea katika mkutano huo, Kamati kuu ya CAF ilikutana na kufikia maamuzi yafuatayo:-

Ukaguzi wa mwisho wa  viwanja nchini Cameroon kuelekea fainali ya bara Afrika mwaka 2019, utafanyika mwishoni mwa mwezi  Novemba na maamuzi kufanyika, hasa kuhusu suala la usalama.

Fainali hiyo itakayokuwa kwa mara ya kwanza na mataifa 24, itafanyika kati ya tarehe 15 mwezi Juni hadi tarehe 13 mwezi Julai 2019.

Aidha, kwa mara nyingine ilithibitishwa kuwa Ethiopia itaanda mashindano ya CHAN mwaka 2020.

Nayo droo ya mashindano ya Afrika kwa vijana wasiozidi miaka 17 nchini Tanzania, mwaka 2019, itafanyika mwezi Desemba mwaka huu.

Timu ambazo zimefuzu ni pamoja na :- Angola, Cameroon, Guinea, Morocco, Nigeria, Uganda, Senegal na Tanzania.

More in