Connect with us

Safari ya kufuzu fainali ya kombe la dunia mwaka 2018 yaanza

Safari ya kufuzu fainali ya kombe la dunia mwaka 2018 yaanza

Mataifa 10 ya Afrika yanashuka dimbani hivi leo kumenyana katika mzunguko wa kwanza kutafuta nafasi ya kufuzu katika mzunguko wa pili ili kusaka nafasi ya kucheza katika mashindano ya dunia mwaka 2018 nchini Urusi.

Taifa Stars ya Tanzania itakuwa katika uwanja wa taifa jijini Dar es salaam kuanzia saa kumi jioni kumenyana na Malawi.

Tanzania wanawategemea sana washambuliaji wake wa Kimataifa Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wanaochezea klabu ya TP Mazembe nchini DRC.

Timu hizi mbili zimekutana mara 43 tangu mwaka 1974 katika historia yao ya soka na Tanzania imeshinda mara 8, Malawi wameshinda mara 14 na nchi hizo mbili zimetoka sare mara 21.

Mchuano huu ni muhimu pia kwa kocha Charles Boniface Mkwasa ambaye ametia saini mkataba wa miaka miwili na Shirikisho la soka nchini Tanzania TFF kuifunza Taifa Stars.

Harambee Stars ya Kenya nayo ipo ugenini kumenyana na Mauritius.

Kenya watakuwa wanamtegemea sana kiungo wa Kati Victor Wanyama anayechezea klabu ya Southampton nchini Uingereza na mshambuliaji matata Michael Olunga anayechezea klabu ya Gor Mahia.

Hata hivyo, macho na masikio ni kwa Sudan Kusini ambayo inaweka historia kwa kushiriki katika michuano hii ya kufuzu katika fainai za kombe ka dunia kwa mara ya kwanza.

Vijana hao kutoka jiji la Juba watakuwa wenyeji wa Mauritania.

Nahodha wa Sudan Kusini Richard Justin Lado amesema wachezaji wenzake wako tayari kwa mpambano wa Jumatano na wana imani ya kupata ushindi.

Siku ya Alhamisi Kesho Sao Tome itakuwa nyumbani kupambana na Ethiopia huku Liberia ikicheza na Guinea Bissau.

Mataifa haya yatarudiana baada ya wiki moja na mshindi kufuzu katika mzunguko wa pili.

Mataifa ya Uganda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Rwanda tayari yamefuzu katika mzunguko wa pili wa michuano hii.

Hatua ya tatu ya kufuzu itakuwa ya makundi, kutakuwa na makundi matano na mshindi wa kila kundi atafuzu katika michuano hiyo ya dunia.

Bedjos Solutions Bondo

Must See

More in