Connect with us

Waziri wa Michezo nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Denis Kambayi ametangaza kusitisha ligi kuu ya soka nchini humo hadi tarehe 14 mwezi Januari mwaka 2017.

Kambayi amesema, serikali imechukua uamuzi huo kutokana na ongezeko la vurugu katika viwanja vya soka na ukosefu wa uaminifu katika ukusanyaji wa mapato wakati kuna mechi uwanjani katika siku za hivi karibuni lakini pia kwa sababu za kisiasa.

Aidha, Waziri huyo amesema kutokarabatiwa kwa vifaa muhimu uwanjani na tabia mbaya ya mashabiki ya kupigana na kuzozana wanapokuwa uwanjani, kumesababisha hatua hii kufikiwa.

Waziri Kambayi amesema atakutana na viongozi wa soka nchini humo kuona namna ya kutatua changamoto hii kabla ya ligi kurejelewa tena katikati ya Januari mwakani.

Mwezi Mei mwaka 2014, watu walipoteza maisha baada mashabiki kupigana jijini Kinshasa wakati wa mchuano kati ya AS Vita Club na TP Mazembe. Pamoja na hilo, inaonekana suala la siasa nchini humo limechangia mashabiki wanaoshabikia upinzani na serikali kuzozana kila wakati wanapokutana uwanjani.

Tahadhari hii pia imechukuliwa kuelekea tarehe 19, siku ambayo wapinzani wanamtaka rais Joseph Kabila aachie madaraka baada ya muhula wake kukamilika.

More in