Connect with us

 

Siku 30 baada ya kuundwa, kamati ya Tarimba ‘imefeli’ na Yanga ya Sanga ‘itayumba’ zaidi msimu ujao…..

Na Baraka Mbolembole

Kujiuzulu rasmi kwa Manji mara baada ya klabu yake kutwaa ubingwa wa tatu mfululizo Mei, 2017 upande wangu kulikja wakati mwafaka sana na naamini Manji alihitaji kuona Yanga inafanikiwa zaidi na aliona hayupo katika ‘umbo’ zuri kusaidia maendeleo ya klabu aipendayo ndio maana alikaa pembeni na kuwapa nafasi uongozi kujaza nafasi yake.

Sanga hayupo tayari kuona nafasi ya Manji inajazwa na mtu mwingine ndio maana kila mara anapojitokeza mahala kuzungumzia mustakabali wa klabu yake haachi kumtaja Manji. Kitendo cha kaimu huyo mwenyekiti wa klabu kutotoa ushirikiano kwa kamati ya muda iliyoundwa kusaidia kiuchumi klabu wakati huu suala la mabadiliko likiwa katika mchakato, ni muendelezo tu wa namna Sanga alivyo.

Kamati ya Abbas Tarimba ambayo iliundwa Juni 10 mwaka huu ili kusaidia pia usajili wa klabu hawajashindwa kufanya hivyo, bali kwa mwezi wote mmoja walikuwa wakikusanya kwanza fedha kutoka mifukoni mwao na katika vyao mbalimbali ndio maana hivi sasa kuna wachezaji kama nahodha msaidizi, Kelvin Yondan, Juma Abdul, Hassan Kessy, Vicent Andrew, Beno Kakolanya wamekubali kusaini mikataba mipya, huku Mrisho Ngassa na Deus Kaseke wakirejeshwa wakitokea Ndanda FC na Singida United.

Pamoja na jitihada zote za Kamati ya Tarimba lakini bado Sanga anamuwaza Manji badala ya kuangaika kama kaimu mwenyekiti kuhakikisha timu inapata maandalizi ya kutosha kuelekea michezo yao minne ya Caf Confederations. Juzi, Sanga alikutana na viongozi wa matawi ya Yanga na akawaambia kuwa ‘Manji ameomba miezi mitatu zaidi kabla ya kurejea klabuni hapo.”

Hii inamaanisha kuwa licha ya kuwepo kwa mchakato wa mabadiliko ya uendeshaji wa klabu kutoka mfumo wa kutegemea wanachama hadi kuingia katika soko la Hisa, Yanga bado haiku tayari kwa sasa si tu kuboresha kikosi chao, bali kupata kambi ya hadhi yao, mishahara ya wachezaji, michuano ya Caf na watakuwa na msimu mwingine mgumu katika ligi kuu kama ‘fikra za Ki-Manji Manji hazitatoka kichwani mwa SDanga’

Sanga anapaswa kwa sasa kuangaika huku na huko ili kupata pesa za kuendeshea klabu wakati akiendelea kumsubiri ‘bwana wake mkubwa’. Tazama, wakati Jumatano ijayo Yanga watakuwa Nairobi kucheza na Gor Mahia FC katika mchezo wa Tatu wa kundi la nne katika michuano ya Caf lakini bado kuna nusu ya wachezaji hawajaanza mazoezi na hawajaanza kwa sababu uongozi umeshindwa kufanyia kazi mahitaji yao.

Kuendelea kusubiri miezi mitatu ya urejeo wa Manji si tatizo, lakini hadi Oktoba ijayo je, huyu Sanga atakuwa ameifikisha Yanga mahala gani? Na nini ambacho Manji anaweza kukifanya wakati huu makampuni yake yakisimamisha uzalishaji? Hata kabla ya mkutano wa Juni mwaka huu, niliwashauri wana-Yanga ni lazima wahakikishe wanamuondoa Sanga kama wanataka kuona klabu yao ikirejea katika tawi lao, hii kwa sababu naamini mtu huyo hakidhi vigezo vya kuwa ‘bosi kubwa’ wa Yanga.

Nasikia katibu mkuu Charles Boniphace Mkwassa anataka kujiuzulu nah ii inatokana na viongozi wenzake wa juu kushindwa kuwa na mkakati ya kuata pesa za kuisaidia klabu kujiendesha wakati huu, na hata Mkwassa hapendezwi na namna Sanga alivyo busy na suala la Manji kuliko kuisaidia klabu wakati huu ikihitaji msaada.

Yanga imeshindwa kusaini wachezaji wapya lakini bado naipongeza kamati ya Tarimba kwa kusaidia kuwabakisha wachezaji wao muhimu waliokuwa wamemaliza mikataba yao. Tarimba anaweza kubwaga manyanga wakati wowote kuanzia sasa na hii inatokea kutokana na Sanga kukwamisha mambo mengi ya kamati hiyo ambayo wakati mwingine inashndwa kuingia mahala kusaka fedha kwa sababu mwenyekiti hatoi ushirikiano.

Tarimba na Kamati yake wameshindwa kufikia malengo ndani ya siku 30 na klabu inaonyesha bado haiku katika ‘umbo zuri’ kuelekea michuano ya Caf wiki ijayo na ligi kuu msimu ujao na yote haya chanzo chake ni Sanga na ‘ndoto zake za kumrejesha Manji-mtu ambaye hayupo tayari.’ Sanga anapenda sana madaraka ndio maana kwa miaka yote nane amekuwa mbele ndani ya Yanga.

Naamini njia pekee ya kuinusuru Yanga kwa sasa japo wamechelewa ni kujiuzulu tu kwa Sanga na kamati yake ya utendaji, vinginevyo mambo yataendelea kuwa si mambo klabuni Yanga msimu ujao.

talking African football

More in African Football