Connect with us

Swahili Stories

Soka Tanzania: Miaka miwili ya uongozi wa Jamal Malinzi, kuna matumaini

Soka Tanzania: Miaka miwili ya uongozi wa Jamal Malinzi, kuna matumaini

Na Victor Abuso,

Rais wa Shirikisho la soka nchini Tanzania TFF Jamal Malinzi anaelekea kutimiza miaka miwili tangu kuchaguliwa kwake katika wadhifa huo mwezi Oktoba mwaka 2013.

Alipoingia madrakani Malinzi aliahidi kazi moja tu, ya kuimarisha na kuinua kiwango cha mchezo wa soka nchini humo na kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa mataifa bora barani Afrika na duniani katika mchezo wa kandanda.

Ndoto kubwa ya Malinzi ni kwa Taifa Stars ambayo mara ya mwisho kufuzu katika michuano ya mataifa bingwa barani Afrika mwaka 1980 wakati michuano hiyo ilipochezwa nchini Nigeria, kufanya hivyo mwaka 2017 nchini Gabon.

Mbali na hilo, kuendelea kuwafanya watanzania kupenda soka na kufika uwanjani kwa wingi wakati wa michuano ya ligi au timu ya taifa inapocheza ni mafanikio ambayo Malinzi na uongozi wake wanaendeleza vema na hivyo kujiongezea kipato.

Kuendelea kwa mchezo wa soka baina ya wanawake imekuwa mojawapo ya malengo makubwa ya uongozi wa Malinzi kuimarisha soka la wanawake kwa kuweka mipango ya miaka mitano ya kuimarisha mchezo huo kote nchini.

Twiga Stars ambayo ndio timu ya taifa ya wanawake imeshiriki katika michuano mbalimbali barani Afrika na mwaka huu imefuzu kushiriki Michezo ya Afrika ‘All African Games’ itakayofanyika Congo Brazzaville, mwezi Septemba .

TFF pia imeweka mikakati ya mpango kazi wa maendeleo kwa vijana kote nchini na kuhakikisha kuwa shule zote 16,000 za msingi zinakuwa na viwanja vya kuchezea mpira wa miguu ili kuanza kunoa vipaji kuanzia umri wa chini.

Mpango mwingine wa muda mfupi ni kwa Malinzi na uongozi wake kuunda timu ya taifa ya vijana itakayoshiriki katika mashindano ya fainali za Afrika umri wa chini ya miaka 17 mwaka 2019.

Pamoja na hayo, TFF imekuwa ikifanya mitihani mbalimbali kwa waamuzi wake ili kuwapandisha madaraja na kuimarisha utendaji wao wanapokuwa uwanjani.

Suala lingine ambalo linawafanyiwa kazi na uongozi huu ni pamoja na kuimarisha uhusiano kati ya TFF na Shirikisho la soka Kisiwani Zanzibar ZFA.

ZFA kwa kipindi kirefu imekuwa ikilalamikia kumezwa na TFF na wakati wa uteuzi wa wachezaji wa timu ya taifa mara nyingi wachezaji kutoka Zanzibar wamekuwa wanadai kutengwa.

Aidha, ZFA imekuwa ikiomba uanachama katika Shirikisho la soka duniani FIFA ili kuwa mwanachama kamili, mazungumzo ambayo TFF inasema inaunga mkono na ni ahadi ambayo Malinzi kabla ya kuchaguliwa kwake aliahidi atahakikisha kuwa FIFA inaitambua Shirikisho hilo.

Licha ya mafanikio hayo yanayoendelea kuonekana katika soka la Tanzania, nidhamu bado ni tatizo si tu kwa wachezaji lakini pia kwa viongozi wa soka nchini humo.

Tabia ya wachezaji kuwavamia waamuzi wakati wa michuano ya ligi kuu linasalia suala tata pamoja na tabia ya baadhi ya mashabiki kukabiliana na kuharibu viti uwanjani kama ilivyoshuhudiwa msimu uliopita wakati wa mpambano kati ya Yanga na Simba katika uwanja wa taifa wa jijini Dar es salaam.

Changamoto nyingine ni wizi wa mapato ya Shirikisho hasa yale ya mlangoni na zaidi ya kesi zaidi ya Hamsini kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita zimeripotiwa lakini washukiwa hawajawahi kufikishwa Mahakamani.

Wapenzi wa soka wanasubiri kuona kazi atakayoifanya Malinzi kwa muda unaosalia kabla ya uchaguzi mwingine kufanyika.

Je, uongozi wake utavunja rekodi na kushuhudia Taifa Stars ikifuzu kucheza katika michuano ya Mataifa bingwa barani Afrika mwaka 2017 nchini Gabon ? Tunasubiri.

 

 

 

 

Appointed by CAF President Dr.Ahmad as CAF Media Expert. An expert on African football with over 13 years experience ,always with an ear to the ground with indepth knowledge of the game. I have worked for top publications including 7 years at www.supersport.com until i founded www.soka25east.com to quench the thirst of football lovers across the continent. I have trained young upcoming journalists who are now a voice in African football.I have covered World Cup,AFCON,CHAN,Champions League,Confederations Cup,Cecafa,Cosafa,Wafu and many other football tournaments across the World. Founder Football Africa Arena(FAA),Founder www.afrisportdigital.com

More in Swahili Stories