Connect with us

 

Saint George Sports Club, inayofahamika pia kama Kedus Giorgis kutoka Ethiopia, ndio klabu pekee kutoka ukanda wa CECAFA eneo la Afrika Mashariki inayoendelea katika harakati za kutafuta ubingwa klabu bingwa barani Afrika.

Ni miongoni mwa vlabu 16 vinavyosubiri droo ya hatua ya makundi siku ya Jumatano kufahamu itamenyana na nani kutafuta kufuzu katika hatua ya mwondoano.

Saint George ilifuzu baada ya kuifunga AC Leopards ya Congo Brazil kwa jumla ya mabao 3-0 baada ya mechi ya nyumbani na ugenini.

Wakicheza ugenini, walipata ushindi mwembamba wa bao 1-0 huku wakipata ushndi wa mabao 2-0 nyumbani jijini Addis Ababa.

Kufikia hatua hii, mshambuliaji wa St.George, Saladin Said anaongoza katika safu ya ufungaji wa mabao katika michuano hii.

Ameifungia klabu yake mabao matano.

Mabingwa hao mara 28 wa soka nchini Ethiopia walianza kushiriki katika michuano ya klabu bingwa Afrika mwaka 1997 na mwaka 2017 ni mara ya 10.

Mwisho ilikuwa ni mwaka 2011 walipoondelewa katika hatua ya awali ya michuano hii na Recreativo Caala ya Angola.

Historia inaeleza kuwa hii ndio mara ya kwanza kwa Saint George kufika katika hatua ya makundi baada ya kutofanikiwa kufanya hivyo mwaka 1997, 2000,2001, 2003, 2004, 2006, 2007, 2010 na 2011.

Katika michuano ya Shirikisho, ni KCCA ya Uganda na Al-Hilal ya Sudan ndio inayosalia katika mapambano ya kutafuta taji hili kutoka upande wa CECAFA.

Hii ndio mara ya kwanza kwa Al-Hilal iliyoanzishwa mwaka 1931 kushiriki katika michuano hii na kufuzu katika hatua hii ya makundi.

Iifuzu katika hatua hii baada ya kuishinda Gambia Ports Authority kwa jumla ya mabao 4-1 baada ya mechi ya nyumbani na ugenini.

KCCA nayo ilifuzu baada ya kuifunga Al-Masry kwa mabao 4-3 kupitia mikwaju ya penalti baada ya sare ya bao 1-1 baada ya mechi mbili.

Mabingwa hawa mara 11 wa ligi kuu ya soka nchini Uganda, inashiriki katika michuano hii kwa mara ya nne sasa, mwaka 1988, 2009, 2014 na sasa 2017.

Wakati huo wote, haijawahi kufuzu katika hatua hii ya makundi.

More in African Football