Connect with us
Raisi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania(TFF) Ndugu Wallace Karia amesema yeyote atakayebainika kufanya vitendo visivyo vya kiungwana kwenye mechi za Ligi Daraja la Kwanza inayoendelea TFF haitasita kuwachukulia hatua.
Rais Karia alisema yapo malalamiko ambayo yanafanyiwa kazi yanayohusu michezo iliyohusisha Dodoma Fc vs Alliance na Biashara Mara vs Pamba ya Mwanza ambapo utaratibu utafuatwa na yeyote atakayebainika hatua dhidi yake zitachukuliwa.
Ameongeza kuwa tayari amemuagiza Kaimu Katibu Mkuu wa TFF Kidao Wilfred kukutana na kamati ya Waamuzi ambao ndio wenye jukumu la masuala yote yanayohusu waamuzi ili kuangalia kama Waamuzi wanaotumika wana uwezo wa kuchezesha kwa kiasi gani.
Aidha Rais Karia amesema TFF inashirikiana na Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa nchini (TAKUKURU) ili kudhibiti vitendo visivyo vya kiungwana na Taasisi hiyo itapatiwa ratiba ya mechi zote ili iweze kufuatilia kwa ukaribu.
Vilevile amesema TFF na Bodi ya Ligi wanashirikiana kwa karibu kuhakikisha anayeshinda ashinde kihalali kwa uwezo akitolea mfano namna mashindano ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) kwa namna yanavyochezeshwa kwa haki na kuleta mvuto.
Amesema ni wakati wa kushirikiana kwa kila mmoja ili mpira uchezwe na kuondoa malalamiko ya kila wakati.

African journalist with passion of football reporting.Also i love politics

More in