Connect with us

 

Timu ya taifa ya soka ya Uganda na ile ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kutoka ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, mwishoni mwa wiki iliyopita, zilijiweka katika nafasi nzuri ya kuendelea kutafuta tiketi ya kufuzu kucheza kombe la dunia  mwaka 2018 nchini Urusi.

Mbali na mataifa hayo mawili, mataifa mengine barani Afrika yalikuwa uwanjani kupambana  kupata ushindi ili kuongeza matumaini ya kufuzu katika michuano hiyo mikubwa duniani.

Uganda 1 Congo-Brazaville 0

Mchuano huu ulichezwa katika uwanja wa Naambole jijini Kampala na kuhudhuriwa na maelfu ya mashabiki wa nyumbani. Licha ya kupoteza mchuano wa Kimataifa wa kirafiki dhidi ya Zambia kwa kufungwa bao 1-0 hivi maajuzi, vijana wa Milutin Micho walijikakamua na kupata ushindi nyumbani.

Bao hilo ushindi lilipatikana katika dakika ya 18 ya mchuano huo, na kutiwa kimyani na mshambuliaji matata Farouk Miya ambaye katika kampeni hii, ameifungia nchi yake mabao 2 hadi sasa.

Ushindi huu umeifanya Uganda kuwa katika nafasi ya pili katika kundi E kwa alama 4 nyuma ya Misri ambayo ina alama 6.

Misri nayo ikicheza nyumbani iliipata ushindi wa kuridhisha wa mabao 2-0 dhidi ya Ghana katika uwanja wa Borg EL Arab mjini Alexandria.

Misri iliandikisha bao lake la kwanza kupitia mkwaju wa penalti uliochanjwa kwa ufasaha na Mohamed Salah  dakika ya 43 kipindi cha kwanza na baadaye Abdallah Said akafunga bao la pili katika dakika ya 86 ya mchuano huo.

Kufungwa kwa Ghana ambayo ni ya nne katika kundi hili kwa alama moja baada ya kutoka sare ya kutofungana na Uganda katika mchuano wa kwanza, kunadidimiza matumaini yake ya kufuzu huku  mara ya mwisho kufuzu katika kombe la dunia ikiwa  ni mwaka 2014 nchini Brazil.

Congo nayo haina alama yoyote na sasa inasubiri kumenyana na Ghana mwezi Agosti mwaka ujao, huku Uganda ikiwa inajiandaa kuikaribisha Misri.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo 2 Guinea 1

Leopard ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imeanza kufufua matumaini ya kufuzu kwa mara nyingine kwa kombe la dunia baada ya kufanya hivyo kwa mara ya kwanza mwaka 1974.

DRC ikicheza ugenini jijini Conakry, ilianza kwa kufungwa baada ya Guinea kupata bao katika kipindi cha kwanza kupitia mshambuliaji Seydouba Soumah.

Hadi kumalizika kwa kipindi cha kwanza, Guinea walikuwa kifua mbele lakini mambo yalikuwa tofauti kipindi cha pili.

Dakika ya 54 ya mchuano huo, Leopard ilisawazisha kupitia Neeskens Kebano na dakika mbili baadaye, dakika ya 56, Yannick Bolasie iliongeza bao lingine na mambo yakamalizika kwa wageni kuondoka na ushindi wa mabao 2-1.

Ushindi huo umeipandisha DRC hadi katika nafasi ya kwanza katika kundi la A kwa alama 6 baada ya michuano miwili. Mchuano wa kwanza iliilaza Libya mabao 4-0.

Tunisia pia ina alama 6 katika kundi hili baada ya kuishinda Libya ugenini, mchuano uliochezwa jijini Algiers nchini Algeria na kuchezeshwa na refarii kutoka nchini Kenya Davies Omweno.

Guinea na Libya hawana alama katika kundi hili, hatua ambayo sasa inafungua ushindani mkali kati ya DRC na Tunisia.

Tunisia watakuwa wenyeji wa DR Congo katika mchuano wa tatu mwezi Agosti mwakani.

Nigeria 3 Algeria 1

Super Eagles ya Nigeria ikicheza nyumbani katika uwanja wa Godswill Akpabio katika jimbo la Uyo, ilipata ushindi mkubwa dhidi ya Algeria ambayo imekuwa ikiorodheshwa na FIFA kama timu bora barani Afrika.

Mataifa haya mawili yalishiriki katika michuano ya kombe la dunia nchini Brazil mwaka 2014, na sasa yanapambana kufuzu tena.

Hata hivyo, matumaini yanaonekana kudidimia kwa upande wa Algeria ambao walishindwa kumdhibiti Victor Moses aliyeifungia Nigeria mabao 2 huku John Obi Mikel naye akiitikisia timu yake nyavu na kuihakikishia nchi yake ushindi huo.

Nigeria ambayo ilishindwa kufuzu katika kombe la mataifa bingwa barani Afrika mwakani nchini Gabon, inaongoza kundi hili kwa alama 6, ikifuatwa na Cameroon ambayo ina alama mbili baada ya kupata alama moja nyumbani dhidi ya Zambia baada ya mchuano wao kumalizika kwa sare ya bao 1-1 mjini Limbe.

Zambia na Algeria wana alama 1 katika kundi hili.

Matokeo mengine :

Kundi C

Mali 0-0 Gabon

Morocco 0-0 Ivory Coast

Kundi D

Afrika Kusini 2-1 Senegal

Cape Verde 0-2 Burkina Faso

Kiongozi wa kila kundi ndiye atakayefuzu katika fainali za kombe la dunia. Afrika itawakilishwa na Mataifa matano.

More in Bafana Bafana (South Africa)