Connect with us

Timu ya taifa ya Uganda na Ivory Coast zimeondolewa katika fainali ya michuano ya mataifa bingwa barani Afrika CHAN, kwa wachezaji wanaocheza soka nyumbani.

Michuano hii inaendelea nchini Morocco na mataifa haya mawili, yamelazimika kuondoka katika michuano hii mapema baada ya kupoteza michuano yao ya pili katika kundi B.

Matokeo haya mabaya, yameyaacha Zambia na Namibia kufuzu katika hatua ya robo fainali kuwania taji hili la tano.

Zambia ilipata ushindi wake wa pili, baada ya kuifunga Ivory Coast mabao 2-1 huku Namibia ikaifunga Uganda bao 1-0 katika dakika za lala salama la mchuano huo katika uwanja wa Marrakech.

Mabao ya Zambia yalitiwa kimyani na Augustine Mulenga, katika kipindi cha kwanza na cha pili cha mchuano huo, na kuihakikishia timu hiyo katika hatua ya mwondoano.

Uganda wakiongozwa na kocha mpya Mfaransa Sebastien Desabre, licha ya kutawala mchezo huo, mambo yalikuwa mabaya pale beki wake Timothy Awany alipooneshwa kadi nyekundu.

Adhabu hiyo ilionekana kuwavunja moyo wachezaji wa Uganda ambao walishindwa kulinda vema lango lao na kusababisha Namibia kupata bao katika dakika ya 92 kupitia mchezaji Panduleni Nekundi.

Mechi ya mwisho, Uganda Cranes watachuana na Ivory Coast katika mechi ya kujaribu kupata ushindi angalau katika mashindano haya kabla ya kurejea jijini Kampala.

Uganda imekuwa na bahati mbaya katika mashindano haya tangu mwaka 2011, 2014 na 2016 na kipindi chote hicho, imeondolewa katika hatua ya makundi.

Morocco na Sudan tayari zimefuzu katika hatua ya robo fainali baada ya kufanya vema katika mechi mbili zilizopita.
Ratiba ya Ijumaa, Januari 19 2018:-

Libya v Nigeria

Rwanda v Equitorial Guinea

Libya ilianza vema baada ya kuishinda Equitorial Guinea mabao 3-0 huku Rwanda na Nigeria zikimaliza mchuano wake wa kwanza bila kufungana.

More in African Football