Connect with us

Paul Manjale,Dar Es Salaam.

WASHAMBULIAJI wageni Amisi Tambwe na Obrey Chirwa wameirejesha timu yao ya Yanga SC kileleni mwa msimamo wa ligi kuu ya soka Tanzania bara baada ya jioni ya leo kufunga mabao mawili ndani ya dakika tano na kuiwezesha miamba hiyo ya mitaa ya Jangwani kuwachapa Maafande wa Tanzania Prisons mabao 2-0 katika mchezo mkali wa ligi hiyo uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar Es Salaam.

Katika mchezo huo uliochezeshwa na mwamuzi,Suleimani Kinugani kutoka Morogoro ilishuhudiwa Yanga SC ikipata bao lake la kwanza kupitia kwa Mrundi Amisi Tambwe aliyefunga kwa kichwa katika dakika ya 70 akiunganisha krosi ya mlinzi wa kulia Juma Abdul Mnyamani aliyekuwa ameingia uwanjani muda mfupi uliopita kuchukua nafasi ya Hassan Kessy Ramadhani.

Dakika tano baadae yaani katika dakika ya 75 Mzambia,Obrey Chirwa aliifungia Yanga SC bao la pili kwa kichwa akiunganisha pasi safi ya kichwa kutoka kwa Amisi Tambwe aliyekuwa akiunganisha krosi safi kutoka wingi ya kushoto kwa Geoffrey Mwashiuya.

Ushindi huo umeifanya Yanga SC sasa kufikisha pointi 59 na kuishusha Simba SC kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.Yanga SC imecheza michezo 26 wakati wapinzani wao Simba SC wakiwa wamecheza michezo 27.Msimamo wa ligi hiyo inaweza kubadilika hapo kesho Jumapili ikiwa Simba SC itaifunga African Lyon kwenye mchezo utakaochezwa kwenye uwanja wa taifa Dar Es Salaam.

African Football Writer contributing @Soka25east | Commentator; appeared on @MySoccerAfrica, @KweseSports, @ntvkenya, others | Keen follower of African Football. E-mail: bonfaceosano@gmail.com

More in