Connect with us

Timu ya soka ya Zanzibar, imeishangaza Rwanda baada ya kuicharaza mabao 3-1 katika michuano wa hatua ya makundi katika michuano ya kuwania ubingwa wa mataifa ya Afrika Mashariki na Kati CECAFA, inayoendelea nchini Kenya.

Amavubi Stars walikwenda katika mchuano huu wa kundi A, wakiwa na matumaini ya kufanya vema baada ya kuanza vibaya kwa kufungwa na Kenya mabao 2-0 Jumapili iliyopita.

Mambo hata hivyo, yaligeuka baada ya wachezaji wa Zanzibar Heroes Mutadhir Yahya, Issa Juma na Kassim Khamis, kutikisa nyavu za Rwanda.

Bao pekee la Rwanda la kufuta machozi lilitiwa kimyani na Muhadjiri Hakizimana katika mchuano huo.

Matokeo haya, yanaifanya Zanzibar kuwa na alama tatu nyuma ya Kenya ambao wana alama nne, baada ya kutofungana na Libya katika mchuano wake wa pili Jumanne jioni mjini Machakos.

Libya inashikilia nafasi ya tatu katika kundi A, kwa alama mbili.

Matokeo haya mabaya kwa Rwanda, yanawafungisha virago katika michuano hii mikubwa katika mataifa ya Afrika Mashariki na Kati.

Ethiopia nayo, imepata matokeo mazuri baada ya kuilaza Sudan Kusini mabao 3-0 katika uwanja wa Bukhungu.

Ushindi huo, unaifanya Ethiopia kuongoza kundi la B kwa alama 3, mbele ya Burundi ambao wana alama 1 sawa na Uganda baada ya kutofungana siku ya Jumatatu.

Mechi zitarejelewa siku ya Alhamisi.

More in