Connect with us

CAF yaifungia timu ya taifa ya vijana ya Uganda

CAF yaifungia timu ya taifa ya vijana ya Uganda

 

Kamati andalizi ya Shirikisho la soka barani Afrika CAF, inayoandaa michuano ya Afrika kwa wachezaji wasiozidi miaka 20 itakayofanyika mwaka ujao nchini Zambia, imeifungia Uganda katika michuano ya kufuzu kwa fainali hiyo kwa kuvunja kanuni za Shirikisho hilo.

Shirikisho la soka nchini Rwanda FERWAFA, linasema limepokea barua kutoka kwa Katibu Mkuu wa CAF Hicham El Amrani kuthibitisha hilo.

Mapema mwezi huu, Rwanda iliilalamikia CAF kuwa Uganda ilimtumia kipa James Aheebwa ambaye alikuwa na umri mkubwa kinyume na kanuni za CAF ambazo zinamtaka mchezaji anayeshiriki katika mashindano hayo awe amezaliwa kuanzia tarehe 1 mwaka 1997.

CAF inasema kuwa kipa huyu alikuwa na pasi mbili za kusafiria, moja inayoonesha kuwa alizaliwa mwaka 1996 huku nyingine ikiwa ya mwaka 1997.

The Hippos ya Uganda inajiunga na Harambee Stars ya Kenya ambayo pia ilifungiwa na CAF kwa kuwachezesha wachezaji waliokuwa na umri mkubwa katika mchuano wake dhidi ya Sudan.

Uamuzi huu wa CAF unamaanisha kuwa Rwanda ambayo ilikuwa imefungwa na Uganda kwa jumla ya mabao 3 kwa 2 baada ya mchuano wa nyumbani na ugenini, sasa itamenyana na Misri katika hatua inayofuata ya kutafuta tiketi hiyo.

 

 

Must See

More in