Connect with us

East Africa

CECAFA: Kenya na Tanzania kumenyana fainali ya wanawake

CECAFA: Kenya na Tanzania kumenyana fainali ya wanawake

 

Kenya na Tanzania zitachuana katika fainali ya kuwania taji la CECAFA kwa mataifa ya Afrika Mashariki na Kati kwa upande wa wanawake siku ya Jumanne juma lijalo.

Harambee Starlets ya Kenya ilikuwa ya kwanza kufuzu baada ya kuishinda Lucy ya Ethiopia katika mchuano wa nusu fainali kwa kuwafunga mabao 3-2, mechi iliyochezwa katika uwanja wa taasisi ya mafunzo ya soka ya Njeru mjini Jinja nchini Uganda.

Hadi kumalizika kwa kipindi cha kwanza, Ethiopia ilikuwa inaongoza kwa bao 1-0, lililotiwa kimyani na mchezaji wa kutegemewa Losa Abera.

Hata hivyo katika kipindi cha pili, Harambee Starlets ilionekana kubadilika na kusawazisha bao hilo kupitia mchezaji wake Nedy Okoth Atieno huku Carolyne Anyango Omondi akifunga bao la pili, huku Mary Kinuthia Wanjiku’ akifunga la tatu katika kipindi hicho.

Losa Abera alirejea tena na kuifungia timu yake bao la pili, lakini muda ulikuwa umekwisha na hivyo kuifanya Kenya ambao ndio mara ya kwanza wameruhusu goli katika michuano hii, kufuzu.

 

95de17a9618b60379e2429eb5aeba7d9_xl

Katika mchuano wa nusu fainali ya pili, Kilimanjaro Queens ya Tanzania bara iliwalemea wenyeji Uganda Crested Cranes kwa kuwafunga mabao 4-1.

Daniel Donisia aliifungia Tanzania bao la kwanza katika dakika ya nne ya mchuao huo, huku Omari Mwanahamisi na Abdalla Stumai wakifunga bao kila mmoja kufikiawakati wa mapumziko ya kufanya matokeo kuwa 3-0.

Kipindi cha pili wenyeji walijaribu kusawazisha lakini mambo yakawa magumu na badala yake Asha Rashid akaipa Tanzania bao la nne, huku Hasifa Nassuna akiipa timu yake ya nyumbani bao la kufutia machozi katika dakika za lala salama la mchuano huo.

Haya ndio mashindano ya kwanza ya CECAFA kwa wanawake kuwahi kufanyika.

Bedjos Solutions Bondo

Must See

More in East Africa