Connect with us

KPL: Gor Mahia Kuendelea Kusaka Ushindi Kuongoza Ligi

KPL: Gor Mahia Kuendelea Kusaka Ushindi Kuongoza Ligi

Na: Victor Abuso

Ligi kuu ya soka nchini Kenya KPL, inaendelea leo Jumapili katika viwanja mbalimbali nchini humo.

Mabingwa watetezi na viongozi wa ligi hiyo Gor Mahia wanachuana na Nakuru All Stars katika uwanja wa taifa wa Nyayo jijini Nairobi.

Gor Mahia wanaofahamika kwa jina maarufu kama Kogalo, hadi sasa wameshinda mechi nane, wametoka sare mara tatu na hawajapoteza mchuano wowote, rekodi ambayo wanalenga kuiendeleza leo Jumapili.

Nakuru All Stars ambao walipandishwa daraja msimu huu wanashikilia nafasi ya mwisho katika msururu wa ligi hiyo kwa alama tatu, kutokana na kupata ushindi mmoja tu kati ya mechi 10 walizocheza.

Mabingwa wa zamani Sofapaka FC nao watakuwa katika uwanja wao wa nyumbani huko mjini Machakos kumenyana na wakata miwa Sony Sugar.

Mathare United nayo inakwaruzana na Western Stima jijini Nairobi, Thika United wapo nyumbani kuwakabili Ulinzi Stars na wanabenki KCB wanakabana koo na Tusker FC katika uwanja wa City jijini Nairobi.

Jana Jumamosi, AFC Leopards walipata ushindi wa mabao 2 kwa 0 dhidi ya Muhoroni Youth na kupanda hadi katika nafasi ya pili katika msururu wa ligi kwa alama 21 baada ya kucheza mechi 12.

Leopards walipata mabao hayo kupitia wachezaji wake Jacob Keli na Jackson Saleh na huu ni ushindi wa tatu mfululizo kwa klabu hii inayofunza na kocha kutoka Croatia Zdravko Logarusic .

Katika matokeo mengine ya michuano ya jana, City Stars ilitoka sare ya bao 1 kwa 1 na Ushuru FC na kujipatia alama moja lakini pia Chemelil wakiwa nyumbani walitoka sare ya bao 1 jwa 1 na Bandari FC kutoka mjini Mombasa.

Ratiba hii inaendelea siku ya Jumatano juma lijalo ambapo Ulinzi Stars wakiwa nyumbani mjini Nakuru, watawakaribisha Mathare United huku Bandari wakiwa nyumbani mjini Mombasa wakichuana na Nakuru All Stars.

Bedjos Solutions Bondo

Must See

More in