Connect with us

Morocco imekuwa nchi ya tatu kutoka ukanda wa Afrika Kaskazini kushinda taji la soka la CHAN barani Afrika kwa wachezaji wanaocheza soka katika ligi za nyumbani.

 Atlas Lions waliingia katika historia hiyo baada ya kuishinda Nigeria mabao 4-0 katika fainali iliyopigwa Jumapili iliyopita mjini Cassablanca.

Pamoja na hilo, Morocco imekuwa nchi ya kwanza kuwa mwenyeji na mshindi wa michuano hii ya CHAN.

Mataifa mengine ya Afrika Kaskazini ambayo yamewahi kushinda taji hili ni pamoja na Tunisia mwaka 2011, wakati michuano hii ilipoandaliwa nchini Sudan.

Tunisia ilishinda fainali hiyo kwa kuifunga Angola mabao 3-0.

Libya nayo iliingia katika historia ya michuano ya CHAN mwaka 2014, wakati michuano hii ilipofanyika nchini Afrika Kusini, na kuwashinda Ghana kwa mabao 4-3 kupitia mikwaju ya penalti.

Michuano ya mwaka 2018 ilishuhudia mataifa mawili ya Afrika Kaskazini yakishiriki katika michuano hii ambayo ni Morocco na Libya.

Tunisia na Algeria ni mataifa mengine ya Afrika Kaskazini ambayo yaliwahi kushiriki katika michuano hii ya CHAN.

Taifa lingine ambalo limewahi kushinda taji hili na linashikilia historia kwa kunyakua taji hili mara mbili mwaka 2009 na 2016 ni Jamhuri ya Kidemokorasia ya Congo.

Mashindano haya yalianza mwaka 2009 nchini Ivory Coast, lengo kubwa likiwa ni kuwapa nafasi wachezaji wanaocheza soka katika ligi za nyumbani, kupambana katika soka la bara Afrika.

Sudan ilikuwa mwenyeji mwaka 2011, Afrika Kusini 2014, Rwanda 2016, Morocco 2018 baada ya kuchukua nafasi ya Kenya iliyoshindwa kutoka na maandalizi mabaya.

Ethiopia itakuwa wenyeji wa michuano hii mwaka 2020.

More in