Connect with us

Urusi 2018: Kenya na Tanzania zafuzu mzunguko wa pili

Urusi 2018: Kenya na Tanzania zafuzu mzunguko wa pili

Tanzania na Kenya zimefuzu katika hatua ya pili ya kutafuta nafasi ya kucheza katika hatua ya makundi kufuzu katika kombe la dunia mwaka 2018 nchini Urusi.

Taifa Stars wakicheza katika uwanja wa Kamuzu Banda mjini Blantyre siku ya Jumapili, walifungwa na wenyeji wao Malawi bao 1 kwa 0 lakini wamefuzu kwa sababu mchuano wa kwanza wakiwa nyumbani jijini Dar es salaam, waliwashinda Malawi mabao 2 kwa 0.

Hii ina maana kuwa sasa Tanzania itamenyana na Algeria katika mzunguko wa pili wa mashindano haya nyumbani na ugenini katikati ya mwezi ujao.

Harambee Stars nayo ikicheza Jumapili, katika uwanja wa Kimataifa wa Kasarani jijini Nairobi, ilitoka sare ya kutofungana na Mauritius na imefuzu kwa sababu ya ushindi wa mabao 5 kwa 2 waliyopata ugenini mapema juma hili.

Kenya sasa itamenyana na Cape Verde katika mzunguko wa pili wa michuano hii.

Ethiopia nayo iliyofungwa na Sao Tome and Principe, katika mchuano wao wa ugenini kwa bao 1 kwa 0 leo wamelipiza kisasi kwa kupata ushindi wa mabao 3 kwa 0.

Ethiopia itachuana na Congo Brazavile.

Matokeo mengine, Madagascar waliwafunga Jamhuri ya Afrika ya Kati mabao 3 kwa 0 wakiwa ugenini, Bostwana wakawashinda Eritrea mabao 2 kwa 0 wakiwa ugenini na Chad iliifunga Siere Leone bao 1 kwa 0.

Mataifa ya Uganda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Rwanda tayari yalikuwa yamefuzu katika mzunguko wa pili wa michuano hii.

DRC itamenyana na mshindi kati ya Ushelisheli na Burundi baada ya mshindi kukutana baada ya timu hizi kukutana siku ya Jumanne juma lijalo.

Rwanda itamenyana na Libya huku Uganda wakipepetana na Togo.

Michuano hii ya mzunguko wa pili itachezwa katikati ya mwezi ujao wa Novemba.

Mataifa 20 yatafuzu katika hatua ya tatu na ya makundi na kila kundi litakuwa na timu nne katika makundi matano na mshindi wa kila kundi baada ya mechi za nyumbani na ugenini atafuzu katika michuano ya kombe la dunia.

Mataifa matano kutoka barani Afrika yaliyofuzu katika mashindano ya kombe la dunia mwaka 2014 nchini Brazil yalikuwa ni pamoja na Algeria, Cameroon, Ghana, Ivory Coast na Nigeria.

Bedjos Solutions Bondo

Must See

More in