Connect with us

Yanga raha baada ya kuichabanga watani wao Simba

Yanga raha baada ya kuichabanga watani wao Simba

Mabingwa watetezi wa ligi kuu ya soka Tanzania bara, Yanga FC wameifunga watani wao wa jadi Simba FC mabao 2 kwa 0 katika mchuano wa kukata na shoka jijini Dar es salaam siku ya Jumamosi.

Ushindi huu umemaliza ukame wa miaka miwili ya Yanga kufungwa na Simba au kutoka sare katika michuano mikubwa kama hii katika ligi ya soka nchini humo.

Bao la kwanza la Yanga lilitiwa kimyani na mshambuliaji wa Kimataifa kutoka nchini Burundi, Hamis Tambwe katika dakika ya 44 kipindi cha kwanza.

Simba walianza vizuri mchuano huo huku washambuliaji Awadh Juma na Hamis Kiiza wakikosa nafasi nyingi za kufunga licha ya kuutawala mchuano huo kipindi cha kwanza.

Kipindi cha pili, timu zote ziliingia kwa nguvu lakini Yanga wakailemea Simba kwa kupata bao la pili kupitia Malimi Busungu katika dakika za mwisho za mchuano huo.

Mbuyu Twite mchezaji wa Yanga aliyekuwa amepata kadi ya njano katika kipindi cha kwanza alipata kadi nyekundu katika dakika za lala salama kwa kupoteza muda.

Nahodha wa Simba Musa Mgosi baada ya mchuano huo alisema refarii Israel Nkongo aliwaonea.

Tumecheza vizuri sana lakini kwa bahati mbaya tu hatujapata ushindi hivi leo, refarii hakuwa upande wetu lakini tutapambana siku nyingine, “ alisema.

Naye nahodha wa Yanga Nadir Haroub ‘Canavaro‘ amewashukuru wachezaji wenzake kwa kuonesha mshikamano na kupata ushindi huo mkubwa.

Kilichotuma ushindi leo hii ni umoja wetu na mshikamano, nawashukuru sana wachezaji wenzangu na mashabiki wote nawatakia Jumamosi njema,” alisema Nadir.

Ni furaha kwa mashabiki wa Yanga katika mitaa ya Jangwani na huzuni kubwa kwa mashabiki wa Simba yenye makao yake mtaa wa Kariakoo.

CHAN 2020 MATCHES

Must See

More in